31 Desemba 2021 - 18:49
Marekani: Tuna wasiwasi kuhusu mafanikio ya roketi ya kubeba satalaiti la Iran

Marekani imetangaza kuwa ina wasiwasi kuhusu mafanikio ya roketi ya kubeba satalaiti katika anga za mbali ya Simorgh nchini Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, jioni ya Alkhamisi ya jana ilitangaza wasiwasi wake juu ya kurushwa kwa roketi ya kubeba satalaiti ya Simorgh nchini Iran, na kudai kuwa itaendelea kufungamana na mazungumzo ya Vienna.

Itakumbukwa kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Iran ilitangaza jana Alkhamisi kuwa imerusha kwa mafanikio roketi ya Simorgh inayotumiwa kupeleka satalaiti katika anga za mbali.

Akitangaza habari hiyo,  msemaji wa Timu ya Anga za Mbali ya Wizara ya Ulinzi ya Iran Sayyid Ahmad Hosseini amesema kuwa, suala la kutengeneza maroketi yenye nguvu za kubeba satalaiti kubwa zaidi katika masafa ya mbali zaidi lilipata nguvu na kuwa moja ya ajenda kuu za wizara hiyo baada ya Iran kupata mafanikio katika kurusha angani satalaiti ndogo kwa kutumia maroketi ya Safir na Ghasedak.

Sayyid Hosseini amesema, sehemu zote zilizohusika na urushaji wa roketi hiyo ya majaribio zimefanya kazi zake vizuri na kufanikiwa kufikia lengo lililokusudiwa.

342/